Serikali imetangaza kuanzia mwakani itaanza kununua mazao yote ya nafaka, ili wakulima nchini wawe na soko la uhakika. Hatua hii inalenga kuweka ushindani wa biashara baada ya kuhodhiwa wa wanunuzi binafsi.
Mazao yatakayonunuliwa kupitia Bodi Mpya ya Mazao
ya Nafaka ni mpunga, maharagwe, karanga, choroko, ulezi, ufuta na
mahindi na kwamba yatanunuliwa kwa bei ya ushindani wa soko mwaka huu.
Mchumi wa bodi hiyo, Edwin Mkwenda, alisema hayo
kwenye maonyesho ya wakulima yanayofanyika kitaifa Viwanja vya Nzuguni,
Dodoma.
Mkwenda alisema tayari Serikali imeikabidhi bodi
hiyo maghala yote yaliyokuwa ya Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC),
ambayo hayakubinafsishwa kwenye kanda saba za nchi ili kutunza mazao
yatakayonunuliwa.
Naye Ofisa Ubora wa Mazao wa Bodi hiyo, Dendego
Abdallah, alisema kuundwa kwa bodi hiyo ni ukombozi kwa wakulima kwani
watakuwa na uhakika wa kupata soko la mazao husika.
Abdallah alisema wafanyakazi wa bodi chini ya
Mkurugenzi Mkuu, Eliampaa Kilanga, imejipanga kuanza biashara rasmi
mwakani na kwamba, wakulima wajiandae kuzalisha mazao hayo kwa wingi
kutokana na kuwapo uhakika wa soko.
Wakati huohuo, Shirika la
kuendeleza Bonde la Mto Rufiji (Rubada), limetenga Sh300 milioni kujenga
kituo cha pili cha kufundisha vijana kilimo cha biashara kwa vitendo
eneo la Ngalimila, wilayani Kilombero.
Ofisa Kilimo wa Rubada, Joseph Lyafwila, alisema
hayo kwenye maonyesho hayo kuelezea mkakati wa Serikali kubadili kilimo
kwa vijana, ili walime kibiashara zaidi kupitia mafunzo ya vitendo.
CHANZO http://www.mwananchi.co.tz/kitaifa/Serikali-kununua--nafaka-zote-nchini/-/1597568/1937656/-/13mbvgmz/-/index.html
CHANZO http://www.mwananchi.co.tz/kitaifa/Serikali-kununua--nafaka-zote-nchini/-/1597568/1937656/-/13mbvgmz/-/index.html
No comments:
Post a Comment