KURASA

Thursday, March 12, 2020

HIZI NDIZO DAWA ZA ASILI KWA KUKU

Madawa ya Asili yatokanayo na Mimea yanasaidia katika Tiba na Kinga za maradhi mbalimbali ya Kuku. Sehemu za mimea zinaweza kuwa: Majani, Magome, Mbegu, Maua au Matunda .

 UMUHIMU WA KUTUMIA TIBA ZENYE ASILI YA MIMEA

1. Hupatikana kwa urahisi.
2. Ni rahisi kutumia.
3. Gharama nafuu.
4. Zinatibu vizuri zikitumika vizuri
5. Hazina madhara.

 BAADHI YA MIMEA INAYOTIBU MARADHI YA KUKU

 1. MWAROBAINI (MAJANI, MIZIZI, MAGOME)

 Hutibu magonjwa yafuatayo:
-Typhoid.
-Kuzuia Kideri.
-Kuhara.
-Mafua.
-Vidonda.

 2. SHUBIRI MWITU (ALOE VERA) LITEMBWE

Chukua majani 3-5 makubwa, katakata na loweka ndani ya maji lita 10 kwa masaa 12 hadi 16. Wape kuku kwa siku 5 hadi 7. Isiyotumika mwaga na tengeneza nyingine baada ya masaa 12.

 Mchanganyiko huu unaweza kutibu:
• Kideri/Mdondo  (inyweshwe kabla kwa ajili ya kinga).
• Homa ya matumbo (Typhoid).
• Mafua Infectious Coryza).
• Kipindupindu cha kuku (Fowl Cholera).

 3. MTAKALANG’ONYO (EUPHORBIA)

Chukua Majani makubwa 3-5, ponda, weka katika lita 10 za maji kwa masaa 12-16, chuja na wape kuku. Isiyotumika mwaga na tengeneza nyingine.

 Mtakalang’onyo utibu:
-Kideri/Mdondo
-Ndui.
-Kuhara damu (Coccidiosis)

 4. MBARIKA (NYONYO)

 Htibu: uvimbe.
Weka majani ya mbarika ndani ya majani ya mgomba kisha weka ndani ya jivu la moto, kisha kanda sehemu yenye uvimbe kwa kutumia majani hayo ya mbarika.

 5. MLONGE

Una vitamini A na C nyingi. Chukua majani ujazo wa mikono miwili. Kisha yapondeponde na kuyaweka katika lita 10 za maji na yaache kwa masaa 12-16, chuja na wape kuku. Isiyotumika mwaga na tengeneza nyingine.

 Mlonge Hutibu:
• Mafua.
• Kideri (inyweshwe kabla kwa ajili ya kukinga)
• Kipindupindu cha kuku (Fowl Cholera).
• Homa ya matumbo
• Ini.

 6. KONFREI

• Ina madini na vitamini nyingi.

 Hutibu: vidonda na majipu.

 7. NDULELE (DUNGURUSI, MAKONDE, TURA/NDULA)

• Majani hutibu minyoo.
• Matunda hutibu vidonda.

 8. MAJANI YA MPAPAI

Chemsha mikono miwili ndani ya maji lita 6 hadi ubakie na lita 1. Poza kisha chuja.

 Hutibu: Minyoo

Pia majani ya mpapai ni dawa ya kutibu kuku Kuharisha namna yoyote.

 Kuandaa: Pata jani moja bichi la mpapai na uliponde ponde lilainike kiasi. Kisha changanya na maji kiasi cha lita mbili na nusu.

 Kutumia (kwa tiba): Kuku wapewe maji hayo wanywe, wasipewe maji mengine kwa ajili ya kunywa kwa siku angalau nne au zaidi.

–Inafaa zaidi kila siku kuwaandalia dawa mpya ili dawa isiharibike.

 Kutumia (kama kinga): – Hata kama kuku hawaharishi, wakizoeshwa kunywa maji yenye majani ya mpapai yaliyopondwa angalau mara tatu kwa wiki watakingwa magonjwa mengi.

 Njia nyingine ya kutumia Mpapai:

Kuandaa na Kutumia:
-Chukua majani ya Mpapai uyatwange upate kisamvu chake kiasi cha lita 1.

–Changanya kisamvu hicho na pumba lita 2.

–Waweza kuongezea maji kidogo na kuwapatia kuku wanaoumwa watumie chakula hicho hadi wapone.

Kama kuku ni wachache, andaa chakula wanachoweza kumaliza kwa siku moja ili kisibakie na kuharibika kabla hawajakimaliza.

 9. MAJANI YA MUEMBE

Majani magao mawili, ponda na chemsha ndani ya lita 6 za maji hadi ibaki lita 1. Wape kwa siku moja.

 Mwembe hutibu:
• Homa ya matumbo.
• Mafua.
• Kinga ya Kideri/Mdondo.

 10. MPERA:
Chemsha majani au mizizi.
 Mpera hutibu:
• Tumbo
• Vidonda na majipu.

 11. MINYAA (CACTUS):
Hii ni aina yenye majani manene hadi kufikia nusu nchi na mapana hadi kufikia upana wa viganja viwili vya mikono. Minyaa hutibu:
• Vidonda.
• Ngozi.
• Uzazi.
 (Angalia inaunguza au kubabua).

 12. PILIPILI KICHAA :
(a) Pondaponda kiasi kisha changanya na maji na wawekee kuku wawe wanakunywa kwa muda wao. Inasemekana inasaidia kutibu Mdondo iwapo kuku watapewa mapema kabla maradhi kuingia).

(b) Chukua pilipili kichaa tano (5)  au pilipili ndefu au mbuzi kama ukikosa zote, twanga weka kwenye maji lita 4,wape baada ya kula. Wape kwa siku 5.

 Hutibu: Mafua ya aina zote.

 13. KITUNGUU THWAUMU:

 Hutibu: Mafua, Typhoid, Kuharisha kinyesi cheupe

Jinsi ya kutumia Unakitwanga kisha uchanganye kwenye maji chuja kwa chujio ili kuondoa nyuzi na uchafu.

Kiwango cha kuwapa kitategemeana na idadi ya kuku. Huu ni ushuhuda wa mfugaji aliewahi kutumia kitunguu swaumu kwa kuku wake.

 Tumia dawa za asili kabla ya ugonjwa haujakomaa.

 Kumbuka chanjo kwa kuku ni muhimu.

No comments: