KURASA

Monday, March 8, 2010

KILIMO CHA UYOGA

Miaka ya karibuni, utaalamu wa kuotesha uyoga umeanza hapa Tanzania baada ya watu kutilia maanani lishe bora ya protini na manufaa mengine ya zao hilo. Kwa kuwa uyoga upo wa aina mbalimbali, usitawishaji wake hutofautiana katika mahitaji yake, ikiwa ni pamoja na hali ya hewa, malighafi za kuoteshea, urahisi wa teknologia ya kuotesha katika mazingira ya Tanzania na soko lake kwa wananchi na katika hotel. Hata hivyo ni wananchi wachache tu wanaojua kilimo cha uyoga.



Uyoga unaozalishwa unafahamika. Aina zinazofaa kwa Tanzania ni zile ambazo hustawi vizuri, kwenye maeneo ya joto la wastani wa nyuzi joto 20C hadi 33C. Kwa mfano uyoga aina ya mamama n.k. Aina hizi za uyoga pia uhitaji hali ya unyevu hewani (moisture) wa kiasi cha asilimia 75%.

UOTESHAJI WA UYOGA
Kabla ya kuanza kuzalisha uyoga inabidi kuwa na chumba chenye paa ambalo litazuia jua, mvua, na vumbi. Chumba hiki kinatakiwa kiwe na sakafu inayohifadhi unyevunyevu pamoja na sehemu ya giza ambayo ni muhimu kwa kuotesha utando wa uyoga. Mkulima
wa kawaida anaweza kutumia kasha kama sehemu ya giza.

Mbegu za uyoga huzalishwa kwenye maabara zenye vifaa vinavyowezesha kuotesha mbegu hizo bila kuchafuliwa au kuchanganyika na vimelea kama bakteria, ukungu au jamii
nyingine za uyoga ambazo haziliwi. Hapa Tanzania hivi sasa maabara hizo zipo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kituo cha utafiti wa kilimo-Uyole na taasisi ya utafiti wa kilimo cha bustani- Tengeru (HORTI
Tengeru, Arusha).


HATUA MUHIMU ZA KUOTESHA UYOGA
Hatua muhimu za kuotesha uyoga baada ya kupata mbegu ni kama ifuatavyo:
Kusanya masalia ya mazao kama vile mabua, majani ya mpunga, ngano, pumba za mpunga au mahindi, masalia ya miwa baada ya kukamua nk. Vitu hivi hutumika kama mali
ghafi kwa kuoteshea uyoga.
Mabua, majani ya mpunga au migomba yakatwe kwa urefu usiozidi sm 6, au urefu wa vidole kwa kutumia panga au kisu.
Loweka mali ghafi kwenye maji ya kawaida kwa muda wa siku nzima (masaa 24).
Kisha yachemshe kwa muda wa saa mbili ili kuua vijidudu pamoja na vimelea vilivyomo.
Ipua na umwage maji yote halafu tandaza kwenye kichanja kisafi ili yapoe bila kuchafuliwa na vumbi au vijidudu.
Kisha jaza mali ghafi hii katika mifuko ya nailoni tayari kwa
kupanda mbegu.

NAMNA YA KUPANDA
Kuna aina mbili za upandaji

AINA YA KWANZA


Chukua mfuko wa nailoni wenye upana wa cm 40 - 45 na kimo cm 75. Weka tabaka la mali ghafi ya kuoteshea yenye kina cha sm 10 katika mfuko halafu tawanya mbegu ya uyoga juu yake. Baada ya kuweka mbegu, weka tena tabaka nyingine ya vioteshea na kuweka
mbegu juu yake. Endelea kuongeza tabaka kwa namna hii mpaka ifike ujazo wa robo tatu ya mfuko.

AINA YA PILI

Changanya malighafi ya kuoteshea (baada ya kuchemshwa na kupoa) na mbegu ya uyoga katika uwiano wa 1: 25 (mbegu : malighafi ya kuoteshea) kwa uyoga aina ya mamama (Pleurotus spp.)Kisha mchanganyiko huo ujazwe katika mifuko ya nailoni mifuko hii
iwe na ukubwa wa cm 20 kwa cm 40 ambamo unaweza kujaza kilo 1 – 1.5 ya mali ghafi ya kuoteshea.

Funga mifuko na toboa matundu kwenye mifuko yenye kipenyo cha cm 1 kwa kila umbali wa cm 6 hadi 10 kwa kila mfuko.Matundu yawe mengi ili kuingiza hewa ya kutosha ndani ya mifuko. Kumbuka uyoga ni kiumbe hai hivyo unahitaji kupumua kama inavyoonekana kwenye picha hapo chini.



MATUNZO
Weka mifuko kwenye chumba cha giza. Kwa mkulima wa kawaida waweza kutumia kasha lisilopitisha mwanga kama chumba cha giza. Acha mifuko humo kwa muda wa siku 14 - 21 bila kufunua ili ukungu mweupe uweze kutanda vizuri.Utando wa uyoga ukishatanda vizuri kwenye mali ghafi ya kuoteshea, hamishia kwenye chumba chenye mwanga na hewa ya kutosha kisicho pigwa na jua. Katika chumba chenye mwanga, mifuko inaweza kuwekwa
kwenye, meza, chanja la waya au miti. Mifuko inaweza pia kuning’inizwa kwenye kamba toka kwenye boriti za paa la chumba hicho. Unatakiwa kudumisha hali ya unyevu kwenye chumba hicho cha mwanga kwa kumwaga maji sakafuni. Ukiona vipando vinakauka
unaweza kunyunyizia maji yaliyochemshwa na kupoa juu ya mifuko mara tatu au zaidi kwa siku. Tumia bomba la mkononi lenye ukubwa wa lita moja kunyunyizia maji.
Tafadhali: usizidishe maji kwani maji yakiwa mengi sana yaweza kuozesha uyoga uliyoanza kuota. Aina nyingi za uyoga huanza kutoa vichwa (pini) siku 2 - 3 baada
ya kuwekwa kwenye mwanga.

UVUNAJI
Uyoga huwa tayari kuchumwa siku tatu baada ya vichwa /pini kuonekana.
Uyoga uvunwe kwa mkono kwa kushika katikati ya shina la uyoga kisha zungusha hadi uyoga ung’oke. Usiondoe kichwa peke yake katika kuvuna uyoga kwani kubakiza shina huzuia uyoga mwingine kutokea. Mkulima anatakiwa ajue soko la uyoga kabla ya kuvuna ili kuepuka gharama za kuhifadhi. Kwani uyoga ukishavunwa unatakiwa uliwe
kabla haujaharibika.

JINSI YA KUHIFADHI
i) Unaweza ukauweka uyoga kwenye mifuko ya karatasi na kuhifadhi kwenye jokofu.
ii) Unaweza ukauanika juani hadi ukauke na kuweka kwenye mifuko ya nailoni liyofungwa vizuri ili isipitishe hewa na unyevu.

SOKO LA UYOGA
i) Watu wengi hupenda uyoga mbichi uliotoka shambani wakati huo huo kama kitoweo, kwa kutumia kama nyama, samaki, au kama kiungo.
ii) Unaweza kuuza uyoga mbichi kwa bei ya shilingi 3000/= hadi 5000/= kwa kilo kwa uyoga aina ya mamama.
Pia unaweza kuuza nje ya nchi ikiwa uyoga wako ni kiasi kikubwa na uko katika viwango vinavyo kubalika kimataifa.



MAMBO YA KUZINGATIA
Uzalishaji wa uyoga huzingatia sana hali ya hewa na vifaa ulivyonavyo, hivyo basi, kabla hujachagua aina ya uyoga unaotaka kupanda pata ushauri kwa wataalamu walio
karibu nawe.

Ukishanunua mbegu, kama hupandi kwa muda huo, hakikisha umehifadhi mbegu hiyo kwenye jokofu. Kama huna jokofu la kuhifadhia, nunua mbegu baada ya kuandaa kila kitu. Hata hivyo, uotaji wa mbegu huwa mzuri kama zitakaa nje ya jokofu kwa siku mbili.

Mbegu za uyoga huwekwa ndani ya chupa yenye ujazo wa mililita 300, waweza kutumia chupa moja katika kupanda kwenye kilo 15 ya mali ghafi ya kuoteshea. Hakikisha
unamaliza mbegu yote iliyo ndani ya chupa kwani ikibaki itapata maambukizo ya vimelea.
Hakikisha unaponunua mbegu iwe ni nyeupe. Mbegu ambayo siyo nyeupe ni dalili za maambukizo ya vimelea vingine na hivyo haifai kwa kupanda.

Hakikisha chumba cha kupandia ni kisafi na hakipati vumbi toka nje ili kuzuia maambukizo ya magonjwa ya uyoga.

Usimwagilie uyoga maji yasiyochemshwa kwani maji hayo mara nyingi si salama. Yaweza kusababisha vimelea vingine kuota, kwani uyoga ni dhaifu kuhimili ushindani wa
vimelea.

Pia waweza kusababisha magonjwa ya uyoga ambayo kutibu kwake kunahitaji kutumia dawa za viwandani ambazo ni sumu na hivyo kusababisha madhara kwa mlaji. Unaweza kupata faida nyingi kutokana na uzalishaji wa uyoga,

FAIDA ZA UYOGA:-
Lishe kama protini inayolingana na ile ipatikanayo kwenye maziwa, samaki na kunde. Pia utapata vitamini B, C, na D, na madini ya joto, phosphoras, chuma na potashi.

Uyoga husadikika kutibu maradhi kama kifua kikuu, kisukari, moyo, shinikizo la damu na figo.

Masalia ya mazao hutumika katika kuzalishia uyoga, na baada ya kilimo cha uyoga yanaweza kutumika kama mbolea asili kwa kilimo cha bustani. Masalia ya kilimo cha uyoga pia hutumika kama chakula cha mifugo kama ng’ombe.

Kilimo hiki huhitaji eneo dogo sana la ardhi na kiasi kidogo cha maji, hivyo hupunguza tatizo la ukosefu wa ardhi na ugomvi katika jamii ambao unatokana na tatizo hilo.

Kilimo hiki ni njia nyepesi ya kutoa ajira kwa familia kutokana na gharama ndogo, teknolojia rahisi inayotumika na pato lake kubwa.

14 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Ahsante kwa darasa hili zuri maana mimi na uyoga ni damudamu.

Anonymous said...

Asante sana kwa post hii, napenda sana uyoga
je kuna namna rahisi ambayo mtu anaweza kuotesha uyoga kwa matumizi ya nyumbani, kwa maelezo yako inahitaji uwe na sehemu maalumu ya kuoteshea ambayo nadhani inaweza kuwa gharama kwa mtu anayehitaji kuotesha uyoga kiasi tu kwa matumizi binafsi, tafadhali nifafanulie hili

Bennet said...

Unaweza kuzalisha hata kidogo tu, lakini sehemu maalum lazima iwepo kwa sababu hii sehemu ni kama shamba lako, kama unastoo yako unaweza kufanya hivyo na wakati huo huo ukiendelea kuhifadhi vitu vingine, tatizo linakuwa kwenye kurekebisha kiasi cha unyevu hewani

Masangu Matondo Nzuzullima (MMN) said...

Bwana Bennet - yaani nimejihisi kama niko kwenye darasa la "Agriculture" enzi zile.

Uyoga umebainika kuwa na faida nyingi sana kiafya na baadhi ya madawa muhimu yamegunduliwa kutokana nao. Aina fulani za uyoga pia zina sumu kali sana ambayo inaweza kuua mtu kwa haraka. Nitahakikishaje kwamba uyoga ninaouotesha si ule wenye sumu? Kidogo nina wasiwasi.

Bennet said...

M.M.Nzuzullima - Kama umepata mbegu zako kutoka katika vyanzo ambavyo si vya uhakika, hapo lazima uwe na wasiwasi, lakini kama umenunua mbegu kutoka katika vyanzo nilivyovitaja au vingine vinavyojulikana wala usiwe na wasiwasi kwa sababu ni aina za uyoga ambao hauna sumu

PRISCA said...

nashukuru sana kaka Bennet kwa shule nzuri niliyoipata hapa. naomba unielekeze mbegu itakayonifaa. mimi ninaishi kisarawe na ninataka nianze kupanda hivi karibuni. Prisca kijallo

Esther Green Thomas said...

Habari za Kazi Kaka,
Natamani kujifunza kwa vitendo namna ya kulima uyoga, naweza pata mafunzo mafupi ya wiki moja au mbili?

Suprise group of company said...

Mimi nipo dodoma, na nimependa kuanza uzalishaji wa uyoga.. Natamani kupata darasa fupi. Magali.paul824@gmail.com

zulfa said...

Nimependa sana hii post,binafsi nataka nijue gharama ya hiki kilimo kwa mtu mwenye ardhi ndogo chini ya hekari moja.Na gharama wa ujenzi wa hicho chumba maalum.Pia soko la njee linahitaji nini vigezo vipi

Unknown said...

Daaaahhh

kaka wa hekima said...
This comment has been removed by the author.
kaka wa hekima said...

Nataka kufaam nilazima nichanganye vituvyote yani majan ya mgomba,pumba na vyote au naweza tumia Majani ya mgomba tuu.

Real Life said...

Nahitaji kulima uyoga unaweza kunipatia connection ya mtu atakaye ni guide mpaka mwisho? My number ni 0713123184

Unknown said...

Ahsante