KURASA

Tuesday, June 19, 2012

KIFA UWONGO - MDUDU HATARI KWA MIKOROSHO


Kifa-uwongo (Mecocorynus loripes),. ni mdudu aina ya “weevil” ambaye hushambulia mashina ya mikorosho hata kufikia hatua ya kuuwa mti mzima. Mdudu huyu huitwa “kifa-uwongo” kwa sababu ya mbinu yake makini anayotumia kujihami. Mara tu aonapo mtu anapita karibu yake, huanguka chini na kujifanya kama amekufa kabisa. Kisha baada ya mtu yule kupita, yeye huamka tena na kuendelea na shughuli zake kama kawaida. Wamakonde humwita mdudu huyu “Nang’ang’ana”, ambapo Wayao nao humwita “Ng’ang’ani.

MAISHA YA KIFA UWONGO
“Kifa-uwongo” kama wadudu wengine, hupitia hatua za yai, “lava” na “buu” kabla ya kuwa mdudu kamili. “Kifa uwongo” kamili aliyekomaa, ana rangi ya kahawia na urefu wa kama sentimita 2. Ana mdomo mrefu uliochongoka (snout) ambao daima anauficha kwa kuulaza kifuani pake. “Lava” wake ni aina ya funza (grab) mweupe, mwenye ngozi ya kukunjamana na kichwa cha rangi ya kahawia mzito (dark brown), yeye  daima huonekana amejikunja kama upinde.

“Kifa uwongo” wa kike hutoboa gamba la mkorosho kwa kutumia mdomo wake mkali, na kutaga yai moja moja. Baada ya mayai kuanguliwa, mafunza huanza kushambulia gamba la mti mara moja. Funza hawa wana midomo mikali kama misumeno, nao wanakula kwa bidii sana gamba la mti. Kadri wanavyokula ndivyo wanavyoongezeka ukubwa pia. Funza akaribiapo kuwa Buu (pupa), hupekecha ndani ya mti (kiasi cha sentimita 2.5 chini ya gamba) na kutengeneza matundu kwa ajili ya maficho ya buu (pupal chambers). Mabuu hujifungia ndani ya matundu hayo na hatimaye hugeuka na kuwa “Kifa uwongo” kamili. Mzunguko wa kutokea yai hadi “Kifa-uwongo” kamili, huchukuwa muda wa miezi sita, ambapo muda wa karibu miezi 2 - 2.5 huwa katika hatua ya mafunza, ambayo ndiyo yenye uharibifu mkubwa. “Kifa-uwongo” kamili ana mabawa na anaweza kuruka kwa nadra toka mti hadi mwingine. Mara nyingi wadudu hawa, huonekana wakidumu katika maeneo ya mashambulizi.  Mashambulizi yanaweza kuchukua muda wa mwaka au miwili katika mti mmoja, ambapo mti wa jirani unaweza kuwa huru kabisa bila mashambulizi!.  Mara nyingi “Kifa-uwongo” hupenda kuhamia mkorosho mwingine baada ya kuua kabisa mkorosho waliouanza kushambulia.

DALILI ZA MASHAMBULIZI
Maeneo ya mashambulizi huonekana wazi wazi hata toka mbali, kwa sababu ya uwepo wa Mchanganyiko wa utomvu na takataka kama za maranda ya seremala ambayo hatimaye hugeuka rangi na kuwa nyeusi.   Rangi ya majani ya mkorosho ulioshambuliwa sana, hubadilika na kuwa njano, kisha hunyauka na hatimaye hukauka. “Kifa-uwongo” hupendelea kushambulia miti mikubwa tu. Utafiti umeonyesha pia kwamba hupendelea miti iliyojeruhiwa kutokana na kukatwa kwa ajili ya ubebeshaji  (top-work) au hata ile ya kupunguzwa matawi. Inasadikika kwamba aidha eneo la jeraha ni rahisi kwa kifa uwongo kutaga mayai yake, au huenda kuna mvuto wa aina yake kutokana na harufu ya utomvu utokao eneo lenye jeraha na kufanya mvuto wa pekee kwa kifa uwongo kushambulia!

MKOROSHO ULIOSHAMBULIWA NA KIFA-UWONGO

JINSI YA KUDHIBITI KIFA UWONGO
Hakuna dawa ambayo inashauriwa kutumika katika kuthibiti wadudu hawa, badala  yake, mkulima mwenyewe anashauriwa kupambana nao ana kwa ana: Mwanzoni mwa mashambulizi. Ukaguzi wa mara kwa mara ufanyike kwa kila mkorosho kukagua mashambulizi hayo. Mara tu baada ya kuona  dalili  za mashambulizi ya wadudu hawa, bandua eneo la mashambulizi kwa kutumia kisu  au upanga na kuwaondoa mafunza wote. Funza akidondoka chini hana uwezo tena  wa kupanda kwenye mti au kufanya mashambulizi. Mabuu waliojifungia kwenye matundu  ya maficho  yao, wanaweza kuuawa kwa kutumia  ncha  kali, kama vile spoku yabaiskeli, ili kuwatoboa wakiwa  ndani  yamashimo yao.  Inashauriwa pia kuwasaka na kuwaua  kila “Kifa  uwongo” kamili (adults) kwa kuwakata vichwa vyao.

MASHAMBULIZI YALIYOKITHIRI
Inashauriwa  kukata na kuchoma moto mikorosho yote iliyoshambuliwa kwa kiwango  cha  hali ya juu, ili kuuwa mabaki ya mayai na funza waliopo

No comments: