KURASA

Tuesday, June 19, 2012

MILIBAGI - MDUDU MHARIBIFU WA MIKOROSHO


UTANGULIZI
Milibagi (Pseudococcus longispinus) ni wadudu waharibifu katika zao la korosho, waliojitokeza kuwa maarufu sana katika miaka ya tisini. Hawa ni wadudu wanaoonekana katika maeneo mengi ulimwenguni, lakini hushamiri na kuleta athari kubwa katika mazingira ya Tropikali. Mnamo mwaka 1990, milibagi walionekana kushambulia mikorosho katika maeneo ya mjini Masasi. Mwaka 1993, walionekana kuenea hadi wilaya za Nachingwea na Tunduru. Hivi leo, wadudu hawa wameenea karibu sehemu nyingi za kanda ya kusini, ingawa mashambulizi makubwa yapo wilayani Masasi, Tunduru, Nachingwea na Liwale.   Milibagi ni moja ya wadudu waharibifu wanaoishi na kuponea mimea. Wadudu hawa hutengeneza utando mweupe (scale) juu ya miili yao kwa ajili ya kinga na kujihami dhidi ya adui zao.

Milibagi huonekana katika mazao ya aina nyingi ikiwa ni pamoja na miembemafuta, mihogo, michungwa, minanasi nk. Pamoja na hivyo, kuna tofauti kati ya milibagi wanaoshambulia hayo mazao mbalimbali. Kwa mfano, milibagi wa mihogo (Phenacoccus manihoti), miembe (Rastrococcus invadens) ni tofauti na wale wa mikoroshoni (P. longispinus). Dalili za Mashambulizi ya Milibagi. Maeneo yaliyoshambuliwa na milibagi huonekana yamefunikwa na weupe weupe ambao ni utando unaofunika miili ya wadudu hao. Mikorosho iliyoshambuliwa sana na milibagi, huonekana kwa mbali kama vile imefukikwa na theluji. Mashambulizi ya Milibagi Milibagi wanaweza kushambulia eneo lolote la mmea kwa njia ya kufyonza. Kwa jinsi hiyo, milibagi huingiza matemate yao  katika maeneo ya mashambulizi na hatimaye huweza kueneza vimelea vya virusi. Milibagi hutoa utomvu mweupe mweupe kama asali na kufunika maeneo ya mashambulizi, hata kufanya mmea usiweze kupata mwanga wa jua vizuri hata kuzuia utengenezaji wa chakula cha mimea (photosynthesis).  Majani yaliyoshambuliwa sana na milibagi, hupukutika hivyo kuathiri uzalishaji. Maua yaliyoshambuliwa mapema na milibagi yanashindwa kuzaa. Korosho zilizoshambuliwa zingali zinakomaa, zinachafuliwa kwa utando na utomvu. 

Korosho hizo yamkini zisafishwe kwa mchanga kabla ya kufikiria kuuzwa, vinginevyo hutengwa katika daraja la pili. Mashambulizi ya milibagi, yanaweza kupunguza uzalishaji kwa kiwango cha asilimia 50% Kustawi kwa Milibagi. Milibagi huonekana kwa wingi wakati wa kiangazi, hasa mwezi Septemba hadi Novemba. Milibagi hupungua sana wakati wa mvua. Inaelekea kwamba mabadiliko ya hali ya hewa ni chanzo kikubwa cha mashambulizi ya milibagi kwenye mimea. Maisha ya Milibagi. Milibagi wa kike hutaga kiasi cha mayai 50-500 kutegemeana na mazingira. Mayai huanguliwa na kutokea Vitambaazi (crawler). Hatua hii ni muhimu kwa usambaaji wa milibagi. Hawa hutambaa mpaka kwenye ncha au vilele vya miti na kujitegeshea miguu yao ili wasambazwe kwa upepo, ndege au wadudu wengine. Binadamu pia wanahusika sana kusambaza wadudu hawa katika hatua hii. Hatua za lava zinazofuata ndizo za ulaji na uharibifu. Milibagi waliokomaa (adults) huwa hawajishughulishi (inactive), huwa hawali chakula na huishi muda mfupi (wiki au mwezi)

KUDHIBITI
Zipo  njia mbili ambazo zinaweza kutumika kudhibiti milibagi:
‰ 
NJIA YA KIBAIOLOJIA
Utafiti umeonesha kwamba  wapo wadudu  wengine ambao wanaweza kushambulia milibagi, kama vile:
 a) Ladibedi bito (Chilocorus spp)
b) Manyigu (Chrysopa spp)

Utafiti umeonesha kwamba idadi ya wadudu hawa mashambani ni ndogo kwa kuweza kudhibiti idadi kubwa ya milibagi. Utafiti wa kina zaidi unafanyika kuona jinsi ya kuwafanya wadudu  hawa waongezeke idadi ili kuweza kuwadhibiti milibagi mikoroshoni.

◊ NJIA YA KUTUMIA MADAWA
Njia pekee inayotumika hivi sasa kuwadhibiti milibagi ni kutumia madawa. Dawa aina ya Selecron 720 EC  ndiyoiliyothibitishwa na utafiti itumike dhidi ya milibagi.

Dawa ya Selecron 720 EC Dawa hii ni ya aina ya maji, inayosambazwa  na kampuni ya Norvatis (Ciba Geigy). Inapulizwa kwa  kutumia mashine za moto  (motorized  blowers) kama vile Maruyama 150DX au Solo
◊ Kiwango cha upuliziaji  ni  mililita  7.1 ya dawa, ndani ya lita 1 ya maji kwa mti mkubwa.
◊ Upuliziaji unaanza mara tu  baada  yakuona  dalili  za mashambulizi yamilibagi. 
◊ Marejeo  ya upuliziaji yafanyike kila baada ya siku 7 – 14 kutegemeana na hali ya mashambulizi yalivyo.

No comments: